Sunday , September 23 2018
Home » Uncategorized » BUNGE KUPEWA TAARIFA YA MAFUTA YA KULA

BUNGE KUPEWA TAARIFA YA MAFUTA YA KULA

Leo saa 11 jioni Serikali inatarajiwa kutoa taarifa bungeni kuhusu uchunguzi uliofanywa kwenye tani 40,000 za mafuta ya kula yanayodaiwa ni ghafi yaliyopo kwenye maghala jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Charles Mwijage jana asubuhi aliahidi kumpa taarifa Spika wa Bunge, Job Ndugai kabla ya saa 11 jioni jana.

Wakati wa kikao cha jioni jana, Mnadhimu Mkuu wa Serikali bungeni, Jenista Mhagama alilieleza Bunge Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikutana na mamlaka zinazohusika kwenye suala hilo na kwamba, leo saa 11 jioni Serikali itatoa taarifa bungeni.

Jana jioni Spika wa Bunge, Ndugai alisema taarifa ya serikali kuhusu suala la mafuta ya kula litakuwa la kwanza kwenye kikao cha leo jioni, na kama serikali isipotoa taarifa hiyo atalimaliza jambo hilo ‘kiaina’ na atawaachia wananchi.

Serikali imelieleza Bunge kuwa, uhaba wa mafuta ya kula uliosababisha kupanda bei umesababishwa na mvutano baina ya mamlaka za Serikali kuhusu suala la kodi.

Wabunge jana walielezwa kuwa, nyaraka za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) zinaonesha kuwa mafuta yaliyopo kwenye ghala ni ghafi, nyaraka za Mkemia Mkuu wa Serikali zinaonesha mafuta hayo ni ghafi lakini Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inasema mafuta hayo si ghafi na si safi kabisa.

Mafuta ghafi yanakatwa kodi asilimia 10, na mafuta yaliyosafishwa yanatozwa kodi 25%.

Jana Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe alisema bungeni kuwa, bei ya mafuta ya kula ya Korie lita 10 ilikuwa imepanda kutoka Sh 23,000/- hadi Sh.40, 000/-.

Kwa mujibu wa Bashe, bei ya mafuta hayo lita 20 ilipanda kutoka Sh. 50,000 hadi Sh. 73,000/-.

Jana asubuhi Spika Ndugai alisema, kwa namna serikali inavyoshughulikia suala la bei ya mafuta ya kula inaifikisha nchi mahali pagumu sana kwa mambo madogo sana.

“Mambo madogo mno, hivi kweli nchi hii leo wale tuliosoma Chemistry pamoja na mimi, hivi kweli kupima , kupima mafuta kujua kama haya ni semi refined (safi kigodo ) ama ni crude (ghafi) hiyo nayo ni rocket science?, kitu cha dakika 15? Watu wanazunguka wanazunguka…”alisema.

About PamojaFM

Check Also

Pwani Kibaha: Kibaka ajisalimisha kituo cha Polisi baada ya mzigo alioiba kumng’ang’ania kichwani

Mkazi wa Mbezi, Dar es salaam, Frank Japhet (23) amelazimika kujisalimisha kituo cha polisi Mlandizi, …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *